Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo ameipongeza Serikali ya Mkoa wa Shinyanga kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga inayojengwa katika Tarafa ya Nindo, kata ya Iselamagazi, Mkoani hapa.
Mhe. Jafo ametoa pongezi hizo mapema leo tarehe 07/12/2019 na kusema kuwa, amefurahishwa hasa na hatua ya ujenzi ilipofikia pamoja na mfumo wa uvunaji wa maji ya mvua uliowekwa.
"Nakupongeza sana Mhe. Mkuu wa Mkoa na timu yako yote kwa usimamizi mzuri lakini niwapongeze na wananchi kwa kutoa eneo na kukubali Hospitali hii ijengwe hapa. Mazingira yanafurahisha kwa sababu hapakuwa hivi kabla, nimeridhika na muonekano tangu nilipokuwa nakuja" amesema Mhe. Jafo.
Jafo amesema kuwa, pamoja na shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa hapo awali kwa ajili ya kukamilisha majengo 8, Serikali itaongeza tena sh. milioni 500 hivi karibuni ili kuongeza majengo mengine.
"Tuliamua kwamba, fedha hii isije tulisubiri majengo ya kwanza yakamilike ili inapokuja awamu ya pili ifanye kazi ya kuongeza majengo mengine" amesisitiza Mhe. Jafo na kuzitaka Halmashauri nyingine waige mfano wa Halmashauri hiyo.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Wilaya , Bw. Bashir Salum amesema majengo nane yamekamilika kwa shilingi Bil. 1.5 ambayo ni jengo la Utawala, Wodi ya akina mama, Maabara, Chumba cha Dawa, Chumba cha chanjo, Jengo la kufulia, Jengo la X - Ray na Jengo la kutunzia maiti.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amemshukuru Mhe. Jafo kwa kutembelea Mkoa na kumuomba afanye ziara tena ili aone baadhi ya miradi ambayo imekamilika kwa kutumia mafundi wenyeji ikiwemo vituo vya Afya na Ofisi za Tarafa.
NIndo - Iselamagazi
Anuani ya posta: 113 Shinyanga
Simu: 0282-986382
Simu: 0282-986382
Baruapepe za watumishi: info@shinyangadc.go.tz/ded@shinyangadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.