Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Bw. Kisena Mabuba amewataka Watendaji wa Kata na Maafisa Kilimo kusimamia ukusanyaji wa mapato na kudhibiti upotevu wa fedha katika maeneo yao ya kazi ili kuiwezesha Serikali kupata mapato. Agizo hilo limetolewa Februari 19, 2024 wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri.
“Kwenye suala la mapato, hatuna aibu, hali ya mapato katika halmashauri yetu ndugu zangu ni mbaya, mtu yeyote anayekiuka utaratibu wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali mkamateni na waelimisheni wananchi wajibu wajibu wao wa kutoa ushuru.....haiwezekana halmashauri yetu kutofanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato.” Alisisitiza
Mabuba amesema haridhishwi na hali ya ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri hiyo na anachukizwa na kitendo cha mashine za kukusanya mapato kutofanya kazi vizuri. Hivyo, ameelekeza ukaguzi wa mashine hizo ili kubaini ambazo hazifanyi kazi vizuri katika ukusanyaji wa mapato na kuchukua hatua stahiki. Vile vile, ameelekeza ununuzi wa mashine mpya za kukusanya mapato ufanyike ili kuendana na mahitaji halisi.
Akiainisha vyanzo vya mapato katika halmshauri hiyo, Bw. Mabuba amesema kuwa halmashauri hiyo pamoja na vyanzo vingine inategemea mapato ya mazao na mifugo. Kila Afisa Kilimo, Afisa Mifugo na Mtendaji Kata asimame kwa nafasi yake na kuhakikisha kuwa mapato ya Serikali hayapotei na kusisitiza kuwa makusanyo yote yawekwe benki kwa wakati bila kucheleweshwa.
Aidha, Mabuba amemwelekeza Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Bw. Edward Maduhu kuhakikisha halmashauri inapata taarifa ya mavuno yanayoanza kuvunwa ili kuweka msisitizo wa ukusanyaji mapato katika maeneo hayo.
Awali akielezea vipaumbele vya halmashauri wakati wa uwasilishaji wa rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwa mwaka 2024/2025, Bw. Mabuba alimweleza Mkuu wa Mkoa Shinyanga kuwa halmashauri hiyo imejipanga kwa kuweka mikakati madhubuti ambayo itasaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Baadhi ya mikakati aliyoiainisha ni pamoja na kufuatilia na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na wa kushtukiza ili kuziba mianya ya wizi, kutoa elimu kwa wafanyabiashara, kuandaa kanzi data ya wafanyabiashara wote, kuwezesha wakusanya mapato kwa kuwapatia vitendea kazi muhimu na kuongeza mashine za kukusanya mapato ( POS).
Baadhi ya Maafisa Kilimo, Maafisa Mifugo na Watendaji Kata wakisikiliza kwa
makini wakati wa kikao kazi.
NIndo - Iselamagazi
Anuani ya posta: 113 Shinyanga
Simu: 0282-986382
Simu: 0282-986382
Baruapepe za watumishi: info@shinyangadc.go.tz/ded@shinyangadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.