Wananchi wilayani Shinyanga wamehimizwa kujiunga kwa wingi na mfuko wa Bima ya Afya ulioboreshwa ili wapate vitambulisho vitakavyowasaidia kupata matibabu kwa mwaka mzima katika vituo vya kutolea huduma za Afya ikiwemo na Hospitali za Rufaa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainab Telack wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya iliyoboreshwa (CHF) katika kijiji cha Ilobashi, kata ya Masengwa, wilayani Shinyanga, ambapo amesema kuwa Bima ya Afya inawasaidia wananchi kuwa na uhakika wa matibabu kwa bei nafuu kwa mwaka mzima.
Amesema kuwa wananchi wakiwa na uhakika wa matibabu, maradhi yakiwakuta hawana fedha hawatakuwa na mawazo ya kwenda kupiga ramli chonganishi kwa sababu tayari wana vitambulisho.
Telack amewaasa pia wananchi ambao vitambulisho vyao vimekwisha muda wake walipie tena kwa mwaka huu ili waendelee kupata matibabu huku akiwakumbusha Waganga wafawidhi wa vituo vyote vya Afya kuhakikisha dawa na vifaa vinakuwepo.
“Serikali inataka Watanzania wote wanakuwa na Bima za Afya ili kuweza kutibiwa kwa wakati, ubora na kwa bei nafuu, hakikisheni madirisha ya wagonjwa wa CHF yanakuwepo na yanafanya kazi kama ilivyo kwa madirisha ya wazee,”amesema Telack
Naye Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga aliyeambatana na Mkuu wa Mkoa katika uzinduzi huo, amewasisitiza wakulima wote kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya mara tu watakapouza pamba ili wawe na uhakika wa matibabu.
NIndo - Iselamagazi
Anuani ya posta: 113 Shinyanga
Simu: 0282-986382
Simu: 0282-986382
Baruapepe za watumishi: info@shinyangadc.go.tz/ded@shinyangadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.