Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wamepata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo uchaguzi wa serikali za mitaa, uhifadhi wa mazingira, uzalendo, ukatili wa kijinsia na fursa za kiuchumi katika kongamano lililoandaliwa eneo la mkesha wa Mwenge wa uhuru Agosti 12, 2024.
Kongamano hilo limefanyika katika uwanja wa stendi ya Salawe na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, taasisi binafsi, wadau kutoka mashirika mbalimbali, wanawake, wazee na wananchi kwa ujumla.
Akizungumza na vijana mara baada ya Mwenge wa Uhuru kuwasili eneo la mkesha, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Godfrey Mnzava, ametoa pongezi kwa halmashauri kufanikisha uwepo wa kongamano hilo na amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kuwa wazalendo ili kuendeleza amani na umoja ndani ya Tanzania.
Awali akiwasilisha mada kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa, Afisa uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Osca Lupavila, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kujiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura ambalo linatarajiwa kuanza hivi karibuni ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu .
Lupavila ametumia nafasi hiyo kutaja sifa za mpiga kura na mgombea, akieleza kuwa lazima mpiga kura anatakiwa awe mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea na awe amejiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Kwa upande wa mgombea anatakiwa awe na umri wa miaka 21 na kuendelea, ajue kusoma na kuandika katika lugha ya kiswahili au kiingereza .
Naye Mwakilishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga Bi. Alicia John, amewataka wananchi kujiepusha na vitendo vya rushwa hasa kipindi cha uchaguzi, akisisitiza kuwa ni jukumu la kila mmoja kuzuia rushwa ili kuwezesha uchaguzi ufanyika kwa haki.
Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru 2024 ni Tunza mazingira na Shiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa taifa endelevu".
NIndo - Iselamagazi
Anuani ya posta: 113 Shinyanga
Simu: 0282-986382
Simu: 0282-986382
Baruapepe za watumishi: info@shinyangadc.go.tz/ded@shinyangadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.