Na. Paul Kasembo, SHINYANGA DC.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha ameipongeza halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga
kwa kupata hati safi na kuitaka Halmashauri hiyo kuitumia vizuri Hati Safi waliyoipata kutekeleza yale yote
yaliyokuwa yamekusudiwa ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) .
Kauli hiyo ameitoa leo Juni 25, 2024 wakati wa mkutano maalum wa Baraza la Madiwani la kupitia na
kujadili taarifa ya hoja za CAG kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Mhe. Macha ametoa pia pongezi kwa halmashauri kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo
ikiwemo ujenzi wa jengo la Utawala ambalo kwa muda kiasi lilisimama ila kwa sasa ujenzi wake unakwenda
kwa kasi sana na umefikia hatua ya umaliziaji . Aidha, ameshauri kuundwa kwa Timu ndogo ya watu watano
(5) ambao watakuwa ni maalum kwa ajili ya kushughulikia na kujibu hoja za CAG peke yake na timu hii iwezeshwe
kikamilifu kwa ajili ya kazi hiyo maalum kwa lengo la kuondoa kabisa hoja zinazojitokeza.
"Pamoja na kuwapongeza kwa kufanya vizuri na hata mkapata hati safi ya CAG, lakini nendeni mkatumie
hati hiyo safi mliyoipata kutekeleza yale yote mliyoyakusudia ikiwemo kutekeleza Ilani ya CCM ambayo
ndiyo inaunda Serikali yetu na ndiyo ambayo ninyi imewaajiri, hivyo zingatieni haya na mkafikie lengo
mlilokusudia na siyo vinginevyo, " amesema Mhe. Macha.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa CAG ndg. Thobias Shija ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Fedha
kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Shinyanga Dkt. Kalekwa Kasanga amesema kuwa Halmashauri
ilikuwa na hoja 35 za mwaka 2022/2023 na hoja za nyuma ni 69 jumla ya hoja 104 ikijumlisha na hoja za nyuma,
ambapo 41 zimejibiwa na kufungwa, 47 zinaendelea na utekelezwaji, zilizofutwa ni 15 na majibu ambayo
hayajakubalika ni moja.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Nicodemus Simoni
amesema kuwa yale yote yaliyoelekezwa na CAG na Mkuu wa Mkoa na yaliyoshauriwa na wajumbe
yamechukuliwa na yatafanyiwa kazi ili ifike wakati waondokane na hoja zote .
NIndo - Iselamagazi
Anuani ya posta: 113 Shinyanga
Simu: 0282-986382
Simu: 0282-986382
Baruapepe za watumishi: info@shinyangadc.go.tz/ded@shinyangadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.