Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Professa Joyce Ndalichako leo Novemba 9,2019 amefanya ziara kwenye halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambapo pamoja na mengine amezindua na kuweka Jiwe la msingi kwenye Majengo ya uthibiti ubora wa Shule.
Kwenye halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, ameweka jiwe la Msingi katika Jengo la Uthibiti ubora katika kata ya Iselamagazi pamoja na kulizindua ambapo limeshakamilika kwa asilimia kubwa.
Akizungumza mara baada ya kukagua jengo hilo na kuweka mawe ya Msingi na kuzindua ,Prof. Ndalichako amewataka wathibiti ubora wa shule kufanya kazi kwa bidii ili kuinua taaluma hapa nchini.
Amesema wathibiti ubora ndiyo kioo cha taaluma hapa nchini, hivyo wanapaswa kuzikagua shule ipasavyo, ili ziweze kutoa elimu bora kwa wanafunzi na kuzalisha taifa la wasomi.
"Serikali ya awamu ya Tano inatumia pesa nyingi sana kwenye sekta ya elimu ili kuhakikisha taifa linakuwa na watu wasomi, hivyo nawaagiza wathibiti ubora wa shule msimamie taaluma ipasavyo," amesema Prof. Ndalichako.
Katika hatua nyingine ameonya kitendo cha wanafunzi kuonyeshwa mitihani ya kuhitimu shule, na kubainisha kuwa yule atakayekamatwa kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Naye Katibu Tawala wa mkoa wa Shinyanga Albert Msovela ,amesema serikali kupitia wizara ya elimu imetoa kiasi cha zaidi ya Shilingi Milioni 600 kujenga Majengo ya Uthibiti ubora katika halmashauri Nne za mkoa wa Shinyanga.
Ametaja halmashauri hizo kuwa ni Kahama Mji, Ushetu, Manispaa ya Shinyanga na halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, ambapo kila Jengo limegharimu Shilingi Milioni 152.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack , amesema kipaumbele cha mkoa huo ni elimu, ambapo watahakikisha kiwango cha ufaulu kinakuwa juu pamoja na wanafunzi kupata elimu bora na siyo bora elimu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Tecknolojia Profesa Joyce Ndalichako, akikagua Ujenzi wa Jengo la Uthibiti ubora wa Shule lililopo Kata ya Iselamagazi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Mthibiti ubora wa Shule halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Joyce Andrew akisoma taarifa ya ujenzi wa Jengo la Uthibiti ubora wa Shule lililopo Kata ya Iselamagazi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
NIndo - Iselamagazi
Anuani ya posta: 113 Shinyanga
Simu: 0282-986382
Simu: 0282-986382
Baruapepe za watumishi: info@shinyangadc.go.tz/ded@shinyangadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.