MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewakumbusha wakulima wa zao la pamba kuacha tabia ya kuchanganya na mazao mengine kwenye shamba moja huku akisisitiza pia juu ya umuhimu mkubwa wa kung'olea maotea kwani tupo nyuma ya wakati.
RC Macha ameyasema haya leo tarehe 9 Novemba, 2024 katika mkutano wa hadhara uliolenga kuwakumbusha wakulima wa pamba katika Kitongoji cha Mwabusiga wilayani Kishapu wakulima ambao pia wamepata elimu na ushauri wa namna bora ya kulima eneo dogo kwa tija zaidi na Balozi wa Pamba nchini ndugu Aggrey Mwanri.
"Ndugu zangu wakulima wa zao la pamba hapa Mwabusiga, niwaombe sana na kuwakumbusha kwa dhati kabisa kuacha tabia ya kuchanganya zao la pamba na mazao mengine katika shamba moja, kwa kufanya hivyo hatutaona mafanikio tarajiwa kutoka kwenye kilimo hiki na hakutakuwa na maana yoyote tena ya kulima pamba," amesema RC Macha.
Awali akitoa hamasa ya kilimo cha pamba Mwanri amesema kuwa tumekuwa tukifanya makosa makubwa sana kuchelewa kung'olea maotea na kuondoa masalia katika zao la pamba kwakuwa madhara yake ni makubwa sana ambapo amesema kwa mujibu wa utaratibu wa kilimo bora masalia na maotea hupaswa kuondolewa kabla ya tarehe 15 / 9 / 2024 na ukichelewa kufanya hivyo unazalisha pamba mapepe na isiyokuwa na ubora.
"Niwaombe sana ndugu zangu Wanabusiga tuendelea kufuata ushauri na maelekezo ya wataalam wetu wa kilimo na wengine ili tuweze kuwa na kilimo bora cha kisasa ambapo utapaswa kulima eneo dogo na lenye kukuletea tija zaidi na tusichanganye mazao katika shamba moja na tung'olee maotea na kuondoa masalia kabla ya kuanza kilimo cha msimu unaofuata," amesema Mwanri.
Aidha ndg. Buluma Kalidusi ambaye ni Mkaguzi wa Pamba Kanda ya Magharibi amewataka wakulima kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za kilimo cha pamba ambapo ndani yake zinawakataza kabisa wakulima kutekeleza kilimo cha pamba kwa ujanjaujanja ikiwa ni pamoja na kuondoa masalia na maotea katika shamba kabla ya msimu mwingine wa kilimo yaani Septemba 15 ya kila mwaka (Sheria Na. 2 ya mwaka 2001 na kanuni zake)
NIndo - Iselamagazi
Anuani ya posta: 113 Shinyanga
Simu: 0282-986382
Simu: 0282-986382
Baruapepe za watumishi: info@shinyangadc.go.tz/ded@shinyangadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.